Rasimu, inasubiri kupitiwa na mwanasheria.
Sera ya Faragha
Imesasishwa: 26 Nov 2026
Sera hii inaeleza jinsi DumaBoost inavyokusanya na kutumia taarifa zako binafsi kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya Tanzania, 2022. Mdhibiti wa taarifa ni Duma Brands (BRELA 544579, TIN 152-980-884), Kijitonyama, Dar es Salaam, Tanzania; wasiliana nasi kupitia support@dumaboost.com.
Taarifa tunazokusanya
- Namba ya simu (kwa malipo, taarifa za oda na kufuatilia).
- Barua pepe na jina, ukiamua kutupa.
- Ukichagua kuingia kwa Google au Apple, tunapokea kitambulisho cha akaunti yako, jina na email unayoshiriki. Tunahifadhi kitambulisho kwa kuingia; hatuhifadhi tokeni za kufikia akaunti yako wala nenosiri lako la Google/Apple.
- Viungo na maelezo unayoweka kwenye oda.
- Taarifa za malipo kutoka kwa mtoa huduma wa malipo (hali, kiasi, mtandao). Hatupokei wala kuhifadhi PIN, nenosiri au namba kamili za kadi.
- Taarifa za kiufundi (anwani ya IP, kivinjari) kwa usalama na kuzuia udanganyifu, pamoja na kumbukumbu ya kuingia kwenye akaunti (muda, IP, aina ya simu/kivinjari). Kumbukumbu hizi za usalama hufutwa baada ya siku 180.
- Ukitumia Studio: maandishi ya CV au barua yako, faili unalopakia (tunasoma maandishi yake tu na hatuhifadhi faili lenyewe), na picha ukiamua kuweka (tunaitengeneza upya na kuondoa taarifa za mahali ilipopigwa).
- Sahihi ya barua (ukichagua kuweka): tunahifadhi picha safi ya sahihi tu (tunaondoa karatasi ya nyuma) kwa ajili ya barua yako, na tunaifuta ukiiondoa au nyaraka ikifutwa.
- Kuongea na AI: sauti yako inageuzwa kuwa maandishi na huduma ya sauti ya browser yako (mfano Google kwenye Chrome/Android au Apple kwenye Safari) kwenye kifaa chako. DumaBoost hairekodi wala haihifadhi sauti yako; tunapokea maandishi tu, na yanatumika kama maandishi uliyoandika.
- Ukibonyeza "Nijulishe": huduma uliyoichagua, ikiunganishwa na akaunti yako.
AI na watoa huduma wa nje
Ukibonyeza vitufe vya AI kwenye Studio, maandishi uliyoandika au faili ulilopakia yanatumwa kwa Anthropic (Marekani), mtoa huduma wa AI tunayemtumia kama mchakataji wa taarifa, ili kuandaa nyaraka yako. Hutumwa tu unapobonyeza kitufe cha AI, na chini ya masharti yasiyoruhusu kuyatumia kufundisha mifumo yao. Usiweke taarifa nyeti zisizohitajika kwenye CV (mfano namba ya NIDA, hali ya afya au ya benki).
Ulinzi wa taarifa zako
Password zinahifadhiwa kwa njia ya hash (hatuzioni), link za siri za nyaraka zinahifadhiwa kama hash, funguo za watoa huduma zimesimbwa (encrypted), tovuti nzima inatumia HTTPS, na wafanyakazi wanaingia kwa uthibitisho wa hatua mbili na ruhusa maalum tu. Nyaraka iliyounganishwa na akaunti inafunguliwa na akaunti hiyo tu. Mafaili kama CV, picha, sahihi, logo na designs yanaweza kuhifadhiwa kwa mtoa huduma wetu wa hifadhi Cloudflare (R2): hifadhi ya siri, iliyosimbwa ikiwa imehifadhiwa na ikisafirishwa, inayofunguliwa tu kwa link za muda mfupi zinazotengenezwa na seva yetu. Tunaweka nakala za akiba ili nyaraka zako zisipotee.
Marejesho na kuunganisha oda na akaunti
Marejesho yanalipwa kwenye salio la DumaBoost. Ukilipa bila akaunti, tunahifadhi rekodi ya marejesho pamoja na namba ya simu uliyolipia. Ukifungua akaunti na kuthibitisha namba hiyo, au ukidai kwa link ya oda yako, tunaunganisha oda hiyo na akaunti yako ili marejesho yaingie kwenye salio lako. Hatutumii taarifa hizi kwa jambo jingine.
Kushiriki CV yako na DumaBoost (chaguo lako)
Unapoanza CV tunakuuliza: “Ndiyo, shiriki CV yangu inisaidie kupata kazi”. Kisanduku kimewekwa tiki tayari na maelezo yapo hapo hapo; ondoa tiki kama hutaki. Ukiacha tiki (au ukiwasha “Waajiri waione CV yangu” baadaye), timu ya DumaBoost inaweza kutumia CV yako kukutafutia kazi na kuonyesha CV yako kamili (pamoja na namba ya simu na barua pepe uliyoweka kwenye CV) kwa mashirika yanayoajiri kupitia DumaBoost, kwa kazi zinazoendana na ujuzi, elimu na uzoefu wako. Tunatumia taarifa zinazohusiana na kazi tu; hatutumii wala hatukusanyi jinsia, umri, dini au kabila kuchagua watu. Hatuuzi taarifa zako kamwe. Unaweza kubadilisha jibu lako wakati wowote kwenye wasifu wako au ndani ya CV; CV yako huondolewa kwenye orodha za wagombea ambazo hazijafikia uamuzi. Tunahifadhi kumbukumbu ya lini na wapi ulisema ndiyo au hapana.
Nyaraka za Studio: muda wa kuhifadhi
Nyaraka zilizolipiwa huhifadhiwa ili uweze kuzipakua tena. Rasimu za wageni ambazo hazijalipiwa na hazijaguswa kwa siku 90 hufutwa pamoja na picha. Unaweza kuomba tufute nyaraka yoyote muda wowote.
Business cards
Taarifa unazoweka kwenye business card (jina, cheo, kampuni, simu, email, website, anuani na mitandao) na logo unayopakia huhifadhiwa na kadi yako. Logo inatengenezwa upya kama PNG (taarifa zilizofichwa kwenye faili zinaondolewa) na nakala yake ya asili inahifadhiwa ili uweze kuwasha au kuzima kuondoa background nyeupe; zote zinafutwa ukifuta rasimu au logo. QR code inabeba tu ulichochagua (namba yako, website, WhatsApp au link). Ukiagiza kuchapisha, nakala ya design, logo na taarifa za kuletewa (jina, simu, mkoa na anuani) zinahifadhiwa pamoja na oda na kushirikishwa na wachapishaji na wasafirishaji wetu kwa ajili ya oda hiyo tu.
Design na Uchapishaji, designers na maelezo ya kazi
Kwa flyers, posters, posts, kadi za mwaliko, vyeti, roll-ups, mabango, stickers na thumbnails tunahifadhi maneno, picha na logo unayoweka (picha zinatengenezwa upya kama JPEG bila taarifa za mahali). Orodha za majina ya vyeti zinatumika kutengeneza vyeti vyako tu. Ukichagua designer halisi, designers wetu wanaona design, maelezo na namba yako ya WhatsApp ili kufanya kazi na kukutumia faili; faili zinahifadhiwa uweze kupakua tena. Maelezo ya kazi maalum (jina, WhatsApp, email ukipenda, kampuni na majibu) yanatumika kukujibu na kukupa bei tu, na yanafutwa ukiomba.
Msaada wa zabuni
Kwa msaada wa zabuni tunakusanya taarifa za kampuni yako, za zabuni, namba yako ya WhatsApp na nyaraka unazopakia (usajili, kodi, leseni, mikataba ya awali, CV, taarifa za fedha). Wataalamu wetu wa zabuni na wasimamizi pekee wanaweza kuzifungua, kwa kazi ya kesi yako tu; zinahifadhiwa kwa siri na hazitolewi kwa washindani. Tunahifadhi kesi na nyaraka zake kwa miezi 12 baada ya kufungwa (zaidi tu ukiomba au sheria ikitaka), kisha tunazifuta.
Kazi zangu (zilizohifadhiwa na nilizoomba)
Ukiwa umeingia na ukahifadhi kazi au zabuni, au ukagusa Omba, tunahifadhi hilo kwenye akaunti yako (tangazo lipi na lini) ili ulipate tena kwenye dashboard yako na uone tarehe yake ya mwisho. Halitolewi kwa waajiri. Unaweza kuondoa kazi uliyohifadhi wakati wowote; orodha inafutwa pamoja na akaunti yako.
Maombi ya kazi kwa email
Ukituma maombi kwa email kupitia DumaBoost, tunatumia CV yako, barua yako na tangazo kuandaa maombi (AI inaweza kutumika kuandika barua au kulinganisha CV; maandishi yanapita kwa mtoa huduma wa AI bila kuhifadhiwa naye kwa mafunzo). Email, CV, barua na vyeti ulivyoambatisha vinatumwa kwa anwani ya tangazo tu, na nakala kwako. Tunahifadhi rekodi ya maombi (kazi, mpokeaji, kichwa, ujumbe, tarehe) kwenye akaunti yako. Rasimu zisizotumwa zinafutwa baada ya siku 30; vyeti ulivyopakia vinafutwa siku 90 baada ya kutuma. Picha zinazopakiwa zinachakatwa upya kama JPEG.
Kuandika matangazo kwa AI
Ukitumia "Andika kwa msaada wa AI" unapotangaza kazi au zabuni, maelezo unayoandika yanatumwa kwa mtoa huduma wetu wa AI (Anthropic, Marekani) kama mchakataji wa taarifa ili kuandaa tangazo, pale tu unapobonyeza kitufe na chini ya masharti yasiyoruhusu kuyatumia kufundisha mifumo yao. Ukichagua "Ongea", browser yako inageuza sauti kuwa maandishi kwenye kifaa chako au kupitia huduma yake (Google au Apple, chini ya masharti yao); hatupokei wala kuhifadhi sauti, ni maneno yanayoonekana kwenye kisanduku tu. Usiweke taarifa binafsi za watafuta kazi kwenye maelezo yako.
Waajiri na wanunuzi wanaotangaza
Nembo za kampuni pembeni ya kazi na zabuni zinawekwa na mwajiri mwenyewe au zinachukuliwa kwenye tovuti rasmi ya taasisi hiyo (ikoni au nembo yake ya umma). Tunahifadhi nakala ndogo tu, au tunaionyesha kwa link kutoka anuani ya taasisi yenyewe au huduma ya nembo (Hunter, logos.hunter.io), na tunaifuta taasisi isipokuwa na matangazo tena. Taasisi inaweza kutuomba kubadilisha au kuondoa nembo yake.
Ukitangaza kazi au zabuni tunakusanya taarifa za taasisi (jina, aina, namba ya usajili, TIN, tovuti, email ya kazi, anuani), jina, cheo na simu ya mtu wa mawasiliano, na hati ya uthibitisho unayopakia. Tunavitumia kukagua kwamba tangazo ni la kweli, kuzuia utapeli na kuwasiliana nawe kuhusu tangazo. Jina la taasisi, tangazo na njia ya kuomba vinachapishwa; namba ya usajili, simu, hati na maelezo ya ukaguzi havichapishwi na vinaonwa na timu yetu tu. Tunavihifadhi muda akaunti yako ipo na kwa miezi 24 baada ya tangazo lako la mwisho (hati za uthibitisho zinafutwa ukiomba au baada ya muda huo). Taarifa za mwajiri aliyezuiwa kwa utapeli zinahifadhiwa ili kuzuia matangazo mapya na zinaweza kutolewa kwa polisi au mamlaka husika. Ukiripoti tangazo, tunahifadhi sababu na maelezo yako; hatuhifadhi anuani yako ya IP, ni alama isiyoweza kurudishwa tu ili ripoti moja ihesabiwe mara moja.
Kukukumbusha kumalizia nyaraka
Ukituomba, tunatumia namba au email uliyoweka kukutumia ujumbe mmoja wenye link ya nyaraka yako, kisha tunaifuta.
Vipimo vya matangazo (Meta)
Ukibofya Ruhusu, tunatumia Meta Pixel (cookies) kupima kama matangazo yetu yanafanya kazi: kurasa ulizofungua, kuanza nyaraka, kupakua na malipo (kiasi tu). Meta inapokea taarifa hizi na anwani yako ya IP. Hatutumii jina, simu wala maudhui ya CV yako. Ukikataa, Pixel haipakiwi. Unaweza kubadilisha chini ya ukurasa muda wowote.
Alama na maoni
Ukipata CV au barua ya maombi, ukituma maombi ya kazi, au oda ikikamilika, unaweza kutupa alama (1 hadi 5) na maoni ukipenda. Tunahifadhi alama hiyo pamoja na oda yako ili kuboresha huduma; wafanyakazi wetu wanaiona. Tunaonyesha maoni yako kwenye tovuti yetu (kwa jina lako la kwanza tu) ukiweka tiki tu kwenye “Mnaweza kuonyesha maoni yangu kwenye DumaBoost”; wastani wa nyota unaonyeshwa bila majina.
Kazi na zabuni
Kutafuta na kusoma kazi na zabuni hakuhitaji akaunti wala taarifa zako. Unapobonyeza Omba tunahesabu tu kwamba tangazo hilo limebonyezwa (bila jina, namba ya simu wala anwani ya IP) ili kujua matangazo yanayopendwa. Ukichagua "Usinionyeshe tena", chaguo hilo linahifadhiwa kwenye kivinjari chako tu (local storage) kwa siku 14. Ukifungua kazi au kubonyeza Omba, tunakumbuka kazi hiyo kwenye kipindi chako (session) tu ili Studio ikuulize kama unataka CV au barua ya kazi hiyo; ukibonyeza "Sio sasa" tunaisahau. Ukianzisha CV au barua kutoka kwenye kazi, jina la kazi, mwajiri na tangazo vinaunganishwa na nyaraka yako ya Studio. Ukibonyeza "Linganisha CV yangu na kazi hii", CV yako na tangazo vinatumwa kwa mtoa huduma wa AI kama ilivyoelezwa hapo juu. Hatuwatumii waajiri taarifa zako; unawatumia wewe mwenyewe kwenye ukurasa wao.
Taarifa kwenye simu na kompyuta (alerts)
Ukiwasha taarifa, browser yako inatupa anwani ya kutuma taarifa (kupitia huduma ya taarifa ya Google, Mozilla, Apple au Microsoft, kutegemea browser) na funguo za usimbaji. Tunahifadhi anwani hiyo, ulichochagua (kazi, zabuni, habari, fani na mikoa), lugha, na akaunti yako kama umeingia (ili upate pia taarifa za oda zako). Ujumbe wenyewe husimbwa kabla ya kutumwa. Hatutumi matangazo; tunatuma taarifa moja kwa saa zaidi na hakuna kati ya saa 4 usiku na saa 12:30 asubuhi. Unaweza kuzima wakati wowote kwenye ukurasa wa Kazi na Zabuni au kwenye mipangilio ya browser; tukiona browser imeacha kupokea, tunafuta anwani hiyo. Wafanyakazi wa DumaBoost wanaweza kupata taarifa za ndani (mfano "akaunti mpya", "oda mpya", "malipo yamepokelewa") zenye jina na sehemu ya namba ya simu ya mteja; zinatumwa kwa njia ileile iliyosimbwa (encrypted) na zinakwenda kwa vifaa vya wafanyakazi walioruhusiwa tu.
Kuhesabu wageni (bila cookies)
Tunahesabu idadi ya watu wanaotembelea tovuti, kurasa walizofungua, walikotoka (mfano Facebook, Google) na kama walitumia simu au kompyuta. Hatutumii cookies kwa hili na hatuhifadhi anwani ya IP, jina wala link kamili: tunahifadhi namba ya siri isiyoweza kurudishwa nyuma ambayo hubadilika kila siku. Taarifa hizi hufutwa baada ya siku 90.
Tunavyozitumia
Kutekeleza oda yako, kuthibitisha malipo, kukutumia taarifa za oda, kujibu maombi ya msaada, kuzuia udanganyifu na kutimiza wajibu wa kisheria na kodi. Hatuuzi taarifa zako.
Tunaowashirikisha
Mtoa huduma wa malipo, watoa huduma wanaotekeleza oda (taarifa zinazohitajika tu), mtoa huduma wa AI (Anthropic, kwa Studio na "Andika kwa msaada wa AI" tu), wachapishaji na wasafirishaji (kwa oda za uchapishaji), watoa huduma wa barua pepe/SMS, na mamlaka pale sheria inapotaka. Baadhi ya watoa huduma wanaweza kuhifadhi taarifa nje ya Tanzania; tunahakikisha kuna ulinzi unaotakiwa kisheria. Watoa huduma tunaotumia sasa: Snippe (malipo ya simu, Tanzania); Hostinger (seva za tovuti na barua pepe, kampuni ya Umoja wa Ulaya); Anthropic (AI, Marekani); Google (ukichagua kuingia kwa Google, Marekani); huduma za arifa za kivinjari chako (Google, Mozilla au Apple) ukiwasha arifa.
Muda wa kuhifadhi
Rekodi za oda na malipo huhifadhiwa kwa muda unaotakiwa na sheria za kodi na biashara, angalau miaka 5 kama Sheria ya Usimamizi wa Kodi, 2015 inavyotaka. Ujumbe wa msaada huhifadhiwa hadi miezi 24.
Sheria ya ulinzi wa taarifa
Tunashughulikia taarifa binafsi chini ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022 ya Tanzania na kanuni zake, kama mdhibiti wa taarifa wa DumaBoost. Tunakusanya kinachohitajika tu kwa kila huduma, tunakitumia kwa malengo yaliyoelezwa hapa, tunakilinda kwa udhibiti wa ufikiaji, usimbaji wa taarifa nyeti, kumbukumbu za ukaguzi na ukaguzi wa usalama wa mara kwa mara, na tunahamisha nje ya Tanzania kwa wachakataji wenye kinga za kutosha tu.
Haki zako
Unaweza kuomba kuona, kurekebisha au kufuta taarifa zako, kupata nakala, kuondoa ridhaa uliyotoa (mfano "Ruhusu waajiri kuona CV yangu" au alerts), au kupinga matumizi fulani, kwa kuwasiliana na support@dumaboost.com. Tunajibu ndani ya siku 30. Usiporidhika, unaweza kulalamika kwa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Tanzania.